Social Icons

Featured Posts

Thursday, 1 March 2018

HALI YA UHARIBIFU WA MISITU HANANG,MKOANI MANYARA INAKUWA KWA KASI KUBWA


Katibu wa CCM Wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara,Teddy Athumani(wa kwanza kutoka kulia)akipitia makabrasha ya mkutano wa baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang kujiridhisha namna watendaji wa Halmashauri wanavyotekeleza ilani ya chama tawala.
 Mbunge wa jimbo la Hanang,Mkoani Manyara,Dk.Mary Nagu (wa pili kutoka kulia) akipitia taarifa ya utoaji mikopo kwa vikundi vya wanawake,vijana na walemavu iliyowasilishwa kwenye mkutano huo na kisha kutaka kufahami shilingi milioni 300 zilizoagizwa kwenye mkutano wa LAC Dodoma zitalipwa lini ili vikundi vya wanawake,vijana na walemavu viweze kunufaika na kujiongezea mitaji yao.
 Mkuu wa wilaya ya Hanang,Sara Msafiri akisisitiza jambo kwenye mkutano wa baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
 Katibu wa vikao vya Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Stevine Yonah(wa kwanza kutoka kushoto) akinukuu maazimio yote ya mkutano wa Baraza hilo ili watendaji waweze kutekeleza kikamilifu maazimio hayo.(Picha zote Na Jumbe Ismailly)
 
 
Na,Jumbe Ismailly HANANG       Machi,01,2018        Mazingir
KUTOKANA na hali ya uharibifu wa misitu katika wilaya ya Hanang kuwa kubwa sana,Mkuu wa wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara,Sara Msafiri ameziagiza kamati za maendeleo za kata kujenga utamaduni wa kujadili katika vikao vyao juu ya hali ya uhifadhi wa misitu katika maeneo yao.
Akitoa agizo hilo kwenye mkutano wa kawaida wa Baraza la kawaida la madiwani wa Halmashauri hiyo,Mkuu wa wilaya huyo aliyataja baadhi ya maeneo ya vijiji vya Lalaji.Balangida na maeneo mengine hali ya mazingira ni mbaya sana.
“Kwa hiyo niwaombe kwamba kamati za maendeleo za kata mjadili na hali ya hifadhi ya misitu na ninazo taarifa za kutosha na nimejirisha wapo viongozi wengine  ni wa kisiasa wanashiriki katika biashara ya kukata miti,kuchoma na kuuza mkaa.”alisisitiza Mkuu huyo wa wilaya.
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya kupitia serikali kuu wameshatoa maagizo kwa watendaji kwamba mtu yeyote tule atakayetaka kukata miti hata kama aliupanda mwenyewe ni lazima apate kibali kutoka kwa Mkuu wa wilaya.
Hata hivyo Sara alisisitiza kwamba ni ukweli usiopingika na alioufanyia uchunguzi wa kina na kujiridhisha kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa,wakiwemo madiwani,wenyeviti wa vijiji,vitongoji na watendaji wanajihusisha na biashara ya kukata micti kuchoma mkaa na kuuza mazao hayo.
Akimpongeza Mkuu huyo wa wilaya,Mbunge wa jimbo la Hanang,Dk.Mary Nagu pamoja na kumpongeza Mkuu wa wilaya kwa jitihada zake za kulinda naa kuhifadhi mazingira,lakini aliweka bayana kuwa kama kuna jambo ambalo haliendi vizzuri katika wilaya hiyo ni suala la mazingira.
Diwani wa kata ya Hanang,mjini Peter Lori alionyesha kutoridhishwa na namna Halmashauri isivyoujali msitu wa hifadhi wa Mreru kwani kwa kipindi kirefu serikali imeitelekeza hifadhi hiyo.
Hata hivyo diwani huyo alifafanua pia kwamba inasemekana hifadhi hiyo ni mapito ya wanyama na kuhoji kwamba ni lini Mkuu wa wilaya hiyo atafikiria msitu wa hifadhi Mreru  utakuwa hifadhi ya Halmashauri ya wilaya hiyo.

Wednesday, 28 February 2018

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII NA WIZARA YA KILIMO, MALIASILI, MIFUGO NA UVUVI YA ZANZIBAR ZAWEKA MKAKATI WA KUIMARISHA MUUNGANO

Tuesday, 27 February 2018

DK. KIGWANGALLA ATOA MIEZI TISA KWA WANANCHI KULIPWA FIDIA WAPISHE HIFADHI YA TAIFA TARANGIRE NA PORI LA AKIBA MKUNGUNERONa Hamza Temba-WMU-Manyara
........................................................................

Serikali italipa fidia na vifuta jasho kwa vitongoji ambavyo vipo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Pori la Akiba Mkungunero ili viweze kupisha maeneo hayo yaendelee kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Kimotorok katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ambao ulihudhuriwa pia na Wakuu wa Wilaya za Simanjiro, Kiteto na Kondoa.

Alisema fidia hiyo italipwa kwa vitongoji viwili vya kijiji cha Irkishbo vya Maasasi na Lumbenek  vilivyopo katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara ambavyo vilikutwa ndani ya Pori la Akiba Mkungunero wakati pori hilo linaanzishwa mwaka 1996 kwa Tangazo la Serikali Na. 307.

"Tutafanya tathmini, tutawaomba wananchi mshirikiane na Serikali ili muweze kulipwa fidia mpelekwe maeneo mengine, jukumu letu sisi ni kugharamia zoezi la tathmini na kulipwa fidia ili muweze kuondoka katika maeneo haya ya hifadhi," alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema kwa upande wa baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kimotorok ambao wameanzisha makazi kimakosa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Pori la Akiba Mkungunero hawatalipwa fidia na badala yake watafanyiwa tathmini na kulipwa kifuta jasho na kupelekwa maeneo mengine.

"Kimsingi ukimkuta mtu yupo katika eneo lako hupaswi kulipa fidia, hapa tumekuwa waungwana na kutumia roho ya kibinadamu, vinginevyo tungeweza kusema leo hapa tusione mtu na tungevunja kwa sababu ni eneo halali la hifadhi na hairuhusiwi kwa mujibu wa sheria mtu kuishi ndani ya hifadhi.

"Kwa sasa hatutatumia nguvu, lakini tukikamilisha zoezi la tathmini tukalipa watu fidia yao, tutatoa muda maalum wa watu kuondoka na watu watapaswa kuondoka, ilimradi tutajiridhisha kwamba tulimtendea haki kila mwananchi anayeishi katika eneo hili," alisema Dk. Kigwangalla.

Akizungumzia moja ya zahanati iliyojengwa ndani ya kitongoji hicho cha Kimotorok ambayo nayo itabomolewa baada ya zoezi la kulipa vifuta jasho, aliiagiza TANAPA kujenga zahanati nyingine katika eneo jipya litakalopangwa Halmashauri husika kwa ajili ya wananchi hao kuhamia.

Alisema zoezi la tathmini pamoja na wananchi kulipwa fidia na vifuta jasho linatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi tisa ijayo kuanzia mwezi Machi, 2018. 

Akizungumzia hatma ya makazi mapya kwa wananchi watakaondolewa kwenye maeneo hayo ya hifadhi, Dk. Kigwangalla ameziagiza Halmashauri husika za Kiteto, Kondoa na Simanjiro kupanga maeneo mengine mbadala ya kuwahamishia wananchi hao punde baada ya kulipwa fidia zao.

Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa linalosimamia Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori inayosimamia Pori la Akiba Mkungunero kusaidia jamii jirani na maeneo hayo ya hifadhi kwa kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi, kuendeleza eneo la malisho na kuchimba mabwawa ya maji ya kunywesha mifugo ili kujenga misingi ya urafiki na ujirani mwema.

Katika hatua nyingine, Dk. Kigwangalla amefuta mipaka ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makame ambayo imeingia kimakosa ndani ya Pori la Akiba Mkungunero na kumuagiza Meneja wa Pori hilo, Emmanuel Bilaso kuweka ulinzi mkali katika eneo hilo.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula alisema watasimamia utekelezaji wa maagizo hayo ya Serikali ili kuhakikisha mgogoro huo wa muda mrefu unapatiwa ufumbuzi. 

Katika ziara hiyo ya siku moja Mkoani Manyara, Waziri Kigwangalla alitembelea na kukagua eneo la Ranchi ya Manyara ambayo pia ni sehemu ya mapito ya wanyamapori,  eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge, Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Pori la Akiba Mkungunero ambapo alitoa maelekezo mbalimbali ya kuboresha maeneo hayo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Herman Batiho kukakua maeneo hifadhi hiyo jana wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani Manyara. 

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akionyeshwa mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na viongozi wa hifadhi hiyo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani Manyara jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Herman Batiho kukakua maeneo ya mapito ya wanayamapori na mipaka ya hifadhi hiyo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani Manyara jana. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Sezaria Makuta wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi katika Kijiji cha Kimotorok mkoani Manyara jana. Wanaoshuhudia kushoto Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magesa.

Monday, 26 February 2018

TEKNOLOJIA MPYA YA KUPAMBANA NA UJANGILI KUTUMIKA


 Maafisa Wanyamapori,  maliasili, ulinzi na uhifadhi wa mazingira katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba ya wanyama ya serikali nchini Wakifuatilia mafunzo ya Namna ya kutumia teknolojia ya Smart kwa njia ya simu na kompyuta kukabiliana na Ujangili na uharibifu wa misitu .Mafunzo yaliyofanyika katika Chuo cha Usimamizi  wa Wanyamapori cha Mweka
 Maafisa Wanyamapori,  maliasili, ulinzi na uhifadhi wa mazingira katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba ya wanyama ya serikali nchini Wakifuatilia mafunzo ya Namna ya kutumia teknolojia ya Smart kwa njia ya simu na kompyuta kukabiliana na Ujangili na uharibifu wa misitu. Mafunzo yaliyofanyika katika Chuo cha Usimamizi  wa Wanyamapori cha Mweka

N a Woinde Shizza,Kilimanjaro

Maafisa Wanyamapori,  maliasili, ulinzi na uhifadhi wa mazingira katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba ya wanyama ya serikali nchini waatanza kutumia teknolojia mpya ya kupambana na ujangili baada ya kubaini maeneo yaliyokithiri na ujangili na uharibifu wa mazingira  kwa kutumia simu na kompyuta ili kuimarisha doria na kudhibiti ujangili.
Maafisa hao walisema kuwa matumizi ya simu  na kompyuta zenye programu ya smart ambayo hutumiwa kuainisha maeneo hatarishi kwa ujangili na uvunaji holela wa miti yanaweza kuwekewa alama maalum za kitaalam na kuimarisha ulinzi zaidi.
Afisa wa chuo  cha usimamizi wa wanyamapori cha Mweka  Rudolf Philemon alisema kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yatasaidia kukabiliana na kupunguza vitendo vya kijangili, uvunaji haramu wa misitu na kurahisisha mbinu za kuwakamata majangili.

Rudolf alisema kuwa kwa kutumia program hiyo ipasavyo inatarajia kupunguza vitendo vya ujangili katika Hifadhi za taifa na mapori ya akiba ili mali asili za taifa ziweze kuwa salama kwa manufaa ya Watanzania wote.
Mhifadhi wa pori la akiba la Ugalla mkoani Tabora  Braka Balagaye alisema programu hiyo pia itasaidia katika kukusanya ushahidi wa matukio mbali mbali ya majangili wanapokamatwa katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na misitu ya serikali ambao unaweza kutumika mahakamani.
“Programu hii itawarahisishia kazi askari wanaofanya doria katika hifadhi kuweza kuifanya doria yao kimkakati na kuzaa matunda kwa kudhibiti ujangili ambao ni tatizo sugu barani Afrika katika hifadhi nyingi” Alisema Baraka
Mkufunzi wa programu hiyo kutoka shirika la uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori (WCS)  kutoka nchini Thailand Antony Lyman alisema, programu hiyo ikitumika ipasavyo ina uwezo mkubwa wa kutokomeza kabisa matukio ya ujangili katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
 
Kwa hisani ya Libeneke la Kaskazini

Sunday, 25 February 2018

WAZIRI KIGWANGALLA ATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA YA ARUSHA, ATUMA SALAMU KWA MUWEKEZAJI ANAECHOCHEA MGOGORO KATIKA HIFADHI HIYO


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na viongozi wa TANAPA alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ausha jana na kukagua shughuli mbalimbali za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua mazingira ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kukagua shughuli mbalimbali za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu. Katikati ni Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA, Martin Loibooki na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Steria Ndaga (kulia). 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia moja ya eneo lenye mgogoro ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha alipotembelea hifadhi hiyo jana na kukagua shughuli mbalimbali za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu. Katikati ni Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA, Martin Loibooki na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Steria Ndaga (kulia). 


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA, Martin Loibooki  alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha jana na kukagua shughuli mbalimbali  za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu. Kulia ni Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Steria Ndaga.
Picha ya pamoja Waziri Kigwangalla na baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA.
Waziri wa Malisili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Uhifadhi wa TANAPA, Martin Loibooki kuhusu Kreta ya Hifadhi ya Ziwa Manyara muda mfupi kabla ya kuhitimisha ziara yake katika hifadhi hiyo jana jioni. (Picha na Hamza Temba-WMU)

Thursday, 22 February 2018

WAZIRI MKUU MAJALIWA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA SIKU YA WANYAMA PORI DUNIANI, MACHI 3,2018

 
Mkurugenzi wa Rafiki Wildlife Foundation Mch, Clement Matwiga (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari  (hawapo pichani) katika kuelekea maadhimisho ya 5 ya siku ya wanyamapori duniani, ambayo yatafanyika Kitaifa Dodoma, March 3, 2018,tumekua bega kwa bega kushirikiana na Wizara kutuamini na ndio waandaaji kwa kushirikiana na wizara ya maliasili,  Kulia ni Afisa Wanyamapori Mkuu Idara ya wanyamapori, Eligi Kimario.(PICHA ZOTE NA KHAMISI MUSSA).
 Afisa Wanyamapori Mkuu Idara ya wanyamapori, Eligi Kimario (kulia), akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya 5 ya siku ya wanyamapori duniani, ambayo yatafanyika Kitaifa Dodoma, March 3, 2018, ambapo Mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa. Kushoto ni   Mkurugenzi wa Rafiki Wildlife Foundation Mch, Clement Matwiga.
Mtendaji Mkuu wa Rafiki Wildlife Foundation, Fancis Lazaro (kulia) akizungumza jambo katika Hafla hiyo, Kushoto ni  Afisa Wanyamapori Mkuu Idara ya wanyamapori, Eligi Kimario.

Afisa Wanyamapori Mkuu Idara ya wanyamapori, Eligi Kimario (kushoto) akizungumza katika hafla hiyo, kuanzia kulia ni mratibu wa  Rafiki Wildlife Foundation,  John Masanja na Mtendaji Mkuu wa Rafiki Wildlife Foundation, Fancis Lazaro.

Wednesday, 21 February 2018

SIKU SABA ALIZOTOA WAZIRI KIGWANGALLA ZAZAA MATUNDA

Wiki chache zilizopita Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla alitoa siku saba kwa polisi kukamata watuhumiwa wa mauaji ya mwanaharakati dhidi ya mauaji tembo Wayne Lotter, pia alitaka nyumba zilizouzwa kinyemela huko Arusha zirudishwe na pia alitoa siku saba kwa wakurugenzi wa kampuni nne za uwindaji kukutana nae Dodoma.
Jana kwenye kipindi cha 360 Waziri Dk. Kigwangalla alitoa maelezo ya kina kuhusu maelekezo aliyotoa na pia kuelezea mikakati mbalimbali ya Wizara yake. Kuhusu mauaji ya Lotter alisema kuwa watuhumiwa walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Alimsifu IGP Sirro kwa ushirikiano na Wizara yake.
Alieleza kuwa Katiba inatambua Waziri kama sehemu ya Serikali na kwamba Polisi wapo ili kusaidia Serikali kutimiza malengo yake. Kuhusu nyumba za Arusha, alieleza kuwa ushahidi unaonyesha wazi kuwa waliotajwa walikuwa wamiliki wao binafsi au kupitia familia zao. Waziri Dk.Kigwangalla alieleza mkakati wa kufungua na kukuza utalii kusini mwa Tanzania.
Alieleza mradi wa regrow ambao utawezesha sekta ya kukua kusini mwa Tanzania. Pia alizung umzia umuhimu wa uhifadhi na kueleza kuwa mto Ruaha kwa sasa unakauka kwa siku 60 wakati wa kiangazi na malengo ni kurejesha hadi kukauka kwa siku 10 tu. Kuhusu kutangaza vivutio, Waziri Dk.Kigwangalla alieleza mkakati wa kutangaza vivutio na pia uanzishwaji wa mwezi wa urithi ambao sio tu utaongeza vivutio vya utalii bali utaenzi tamaduni na mila za Kitanzania.

Tuesday, 20 February 2018

DKT. KIGWANGALLA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA BODI YA UTALII (TTB) Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na uongozi wa bodi hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza mapema leo tarehe 20 Februari, 2018.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
...........................................................................

Waziri wa Maliasili na Utaliii, Dkt. Hamisi Kigwangalla leo Februari 20, 2018, amefanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Makao makuu ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jijini Dar es Salaam na kuitaka kufanya kazi kwa kasi na ubunifu zaidi.

Akizungumza na viongozi wa Bodi hiyo, Dkt. kigwangalla amewataka kuongeza kasi zaidi katika kutangaza Utalii wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kuanzisha studio ya kimataifa ya kutangaza vivutio vya Tanzania ndani na nje ya nchi kwa kutumia lugha mbalimbali za Kimataifa.

Aidha,amewataka kuharakisha zoezi la uwekaji wa mabango yanayotangaza Utalii wa Tanzania katika viwanja vya ndege hususani uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam (JNIA).

Hata hivyo amewataka pia kujikita zaidi katika matumizi ya mitandao ya kijamii kwa kuhakikisha inahuishwa mara kwa mara.

Pamoja na hayo, ameiagiza bodi hiyo, kushirikisha wadau mbalimbali wanaotoa huduma za Utalii ikiwemo madereva taxi na Marubani kwa kuwapa elimu ya kutangaza utambulisho wa Tanzania kupitia Utalii na vivutio vilivyopo.

Akiwa katika ofisi hizo ndani ya jengo la Utalii House, alikagua ofisi mbalimbali za bodi hiyo pamoja na zile za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na kupata maelezo machache kutoka wa maafisa wa Shirika hilo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na uongozi wa bodi hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza mapema leo tarehe 20 Februari, 2018.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Devetha Mdachi kukagua mazingira ya ofisi hiyo mapema leo tarehe 20 Februari, 2018.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Devetha Mdachi kukagua mazingira ya ofisi hiyo mapema leo tarehe 20 Februari, 2018.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na uongozi wa bodi hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza mapema leo tarehe 20 Februari, 2018.

Wednesday, 14 February 2018

HIFADHI YA MIKUMI YAIOMBA SERIKALI KUCHEPUSHA BARABARA YA LAMI INAYOPITA NDANI YA HIFADHI HIYONa Hamza Temba-WMU-Morogoro
................................................................
Serikali inafikiria namna bora ya kubadilisha uelekeo wa eneo la kilometa hamsini za barabara ya lami inayopita ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi au kutoza kodi ya utalii kwa watu wanaotumia barabara hiyo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazosabishwa na barabara hiyo kwenye uhifadhi.

Hayo yamesemwa mkoani Morogoro na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla kufuatia ombi la uongozi wa hifadhi hiyo la kuiomba Serikali kuchepusha barabara hiyo kutokana na athari mbalimbali za kimazingira zinazosabishwa na uwepo wa barabara hiyo ndani ya hifadhi hususan vifo vya mara kwa mara vya wanyamapori, ujangili na ukosefu wa mapato ya Serikali.

Awali akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo mbele ya Waziri Kigwangalla, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Gerald Mono alisema licha ya barabara hiyo kuwa na fursa nyingi za kimaendeleo imekuwa na changamoto nyingi kwenye uendeshaji wa shughuli za uhifadhi.

Alisema wastani wa mnyamapori mmoja hugongwa na gari kila siku katika barabara hiyo ambapo takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2014 idadi ya wanyamapori waliogongwa walikuwa 351, mwaka 2015 walikuwa 361 na mwaka 2016 walikuwa 218.

Alisema changamoto nyingine ni uchafuzi wa mazingira ambapo wastani wa taka ngumu zisizopungua kilo 138.3 huzalishwa kila siku na watumiaji wa barabara hiyo.

Mbali na changamoto hizo alisema nyingine ni ukosefu wa mapato ya Serikali kufuatia kukosekana kwa mageti ya kulipia tozo za utalii kwa watumiaji wa barabara hiyo ambao hufaidi utalii wa bure na kuikosesha Serikali mapato.

Alisema Changamoto nyingine ni ujangili ambao huchochewa na uwepo wa barabara hiyo ambayo hutoa fursa kwa majangili kuingia katika hifadhi hiyo kiurahisi kwa njia mbalimbali ikiwemo magari na pikipiki.

“Hifadhi inaiomba Serikali kuchepusha barabara hii ili kupunguza changamoto hizi zinazotokana na uwepo wa barabara husika na kuongeza mapato ya Hifadhi kwa kuzuia utalii a bure unaofanywa na watumiaji wa barabara wa ndani na nje,”. Alisema Kaimu Mhifadhi Mkuu huyo wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alisema changamoto kubwa aliyoiona katika hifadhi hiyo ni namna ya watalii kufika na kufanya shughuli za utalii katika hifadhi hiyo.

Alisema licha ya uwepo wa barabara ya lami inayokatiza hifadhini hapo, barabara hiyo sio rafiki kwenye uhifadhi. “Kuna hiyo barabara ambayo inaleta watalii hapa, ni barabara ambayo iko bize sana, ni barabara ya kitaifa na kwa vyovyote vile hii sio barabara mahsusi kwa ajili ya shughuli za utalii.

“Sisi (Serikali) tunatafakari namna ya aidha kuiondoa hiyo barabara au namna ya kuwachaji watu wanaokatiza hizi kilometa hamsini ambazo zipo ndani ya hifadhi ya Mikumi,” alisema Dk. Kigwangalla.

Katika hatua nyingine Dk. Kigwangalla amemtaka muwekezaji aliyepewa hoteli ya kitalii ya Mikumi Wildlife Lodge iliyopo ndani ya hifadhi hiyo kwa ajili ukarabati na uendelezaji kuhakikisha anakamilisha makubaliano hayo ndani ya muda aliyopewa kwa mujibu wa mkataba aliosaini na TANAPA ama sivyo atanyang’anywa kibali hicho.

Akizungumzia jitihada za kuimarisha ulinzi wa hifadhi hiyo, Dk. Kigwangalla amesema Serikali inakusudia kuharakisha mchakato wa kuanzishwa kwa jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Kidoma itakayojumuisha vijiji vya Kilangali, Doma na Maharaka ili kutengeneza buffer na hatimaye kuimarisha uhifadhi shirikishi.

Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ilianzishwa mwaka 1964 kwa Tangazo la Serikali Na. 465 ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 1,070. Mwaka 1975 Serikali iliona umuhimu wa kuongeza eneo upande wa kusini na kaskazini mwa Hifadhi na kufikia ukubwa wa kilometa za mraba 3,230 kwa tangazo la Serikali Na. 121.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongea na Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Gerald Mono wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi hiyo jana mkoani Morogoro. Uongozi wa hifadhi hiyo umeiomba Serikali kuchepusha barabara ya lami inayopita ndani ya hifadhi hiyo kutokana na athari mbalimbali za kimazingira zinazosabishwa na barabara hiyo ikiwemo vifo vya wanyamapori, ujangili na ukosefu wa mapato ya Serikali unaotokana na watu kufaidi utalii wa bure. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua maziringira ya jengo lililoungua moto la Mikumi Wildlife Lodge ambalo linalofanyiwa ukarabati wakati wa ziara yake ya kikazi katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi jana mkoani Morogoro ambapo amemtaka muwekezaji aliyepewa hoteli hiyo kuikarabati ndani ya muda aliopewa ama sivyo atanyang’anywa kibali alichepewa. Kushoto kwake ni Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Gerald Mono. 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa  na Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Gerald Mono kukagua mazingira ya hifadhi hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi hiyo jana mkoani Morogoro. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipata maelezo  kutoka kwa Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Gerald Mono wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi hiyo jana mkoani Morogoro.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia mazingira mwanana ya  Hifadhi ya Taifa ya Mikumi wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi hiyo jana mkoani Morogoro.
Picha ya pamoja.