Social Icons

Wednesday, 20 November 2013

PORI LA UGALLA HAZINA YA MBWA MWITU TANZANIA


Pori la Akiba la Ugalla lipo upande wa Magharibi mwa Tanzania na jina hilo la Ugalla lilipatikana kutokana na mto maarufu unaotililisha maji yake katika mto Malagalasi na hatimaye kumwaga maji hayo katika Ziwa Tanganyika.

Ukizungumzia mbwa mwitu katika maeneo ya kuhifadhi Wanyamapori moja kwa moja utataja Pori hilo la Akiba Ugalla.Wanyama hawa ambao wana tabia ya kustajaabisha hasa katika utaratibu wao wa mawindo na uzazi ni kivutio cha pekee uwapo ukanda huo wa uhifadhi.

Mbwa mwitu hutembea katika makundi makubwa ya kuanzia ishirini hadi kundi la mbwa mwitu sitini.Kisayansi inaaminika kwamba mbwa hao kutembea katika makundi ni mbinu mahususi ya kujilinda dhidi ya maadui na pia ni mkakati ambao huwawezesha Wanyama hawa kwanza kuona mawindo na kuweza kukamata kiurahisi.Muda wao mzuri kwa mawindo Wanyama hawa ni majira ya asubuhi na jioni mara chache nyakati za mchana siku ambazo hali ya hewa ni mawingu.Wanyama adimu hawa wana mtindo wa pekee wawapo mawindoni ambazo ukizishuhudia kwa macho zinastajabisha sana na kufurahisha.

Wawapo mawindoni wanyama hawa hufukuza windo lao kwa mtindo wa kupokezana yaani kundi la kwanza hufukuza na baada ya muda kundi lingine hupokea na kufukuza windo hilo.Mara baada ya kumfikia kila mbwa hunyofoa mnofu wa windo lao huku wakiwa wanafukuza windo hilo.Mbwa alienyofoa windo hilo hula kipande hicho cha mnofu na kisha huendelea kufukuza mpaka mnyama huyo atakapoanguka na inaaminika mnyama mwenye ukubwa wa swala huweza kushambuliwa ndani ya dakika kumi hadi kumi na tano tu.

Uzazi wa wanyama hawa adimu ni kivutio kingine kinachafurahisha zaidi na sababu hiyo ndio maana wanakuwa wanyama adimu sana na kuendelea kupungua siku hadi siku.Kwani katika kundi moja la mbwa mwitu ambalo hufahamika kama familia huongozwa na jike mkubwa katika kundi hilo yaani "Alfa Female" jike huyo ndie tu anaeweza kuzaa katika kila msimu wa uzazi "Breeding season" ambayo hutokea mara moja kwa mwaka.Jike huyu pia ndiye ambaye huchagua dume wa kumpanda na hivyo hata kama kuna kundi kubwa la mbwa themanini ni jike mmoja tu ambaye ni mkubwa kundini huweza kuzaa kwa msimu mmoja wa uzazi.

Aidha,mbali na Pori la Akiba Ugalla kuwa ni bustani ya mfano kwa Mbwa mwitu,Pori hilo pia ambali ya kuwa na wanyama wengine ni maarufu sana kwa kuwa na Mamba wengi sana hususani katika mto uliozaa jina la pori hilo yaani Ugalla.

Utalii hususani wa wanyamapori na ndege ni moja ya vyanzo muhimu vya mapato ya nchi yetu.

TUSHIRIKIANE KUWALINDA WANYAMA NA KUYALINDA MAZINGIRA.

No comments:

Post a Comment