Social Icons

Wednesday, 20 November 2013

VIONGOZI WA DINI NCHINI WAJITOKEZA KUSHIRIKIANA NA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KATIKA UHIFADHI


 
Viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali nchini, leo wamekutana na Waziri Khamis Kagasheki pamoja na timu ya menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kujadili nafasi ya viongozi wa dini katika kuhamasisha uhifadhi wa maliasili nchini.

Akiwakaribisha viongozi hao wa dini, Mhe Balozi Kagasheki amesifu uamuzi waliochukua wa kutambua umuhimu wao katika kubadilisha mitazamo ya wananchi kupitia mafundisho ya dini.

Askofu Munga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ambaye ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa viongozi wa dini waliotembelea ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii alisema wameona umuhimu wa kujumuika pamoja na Serikali katika kulinda rasilimali za maliasili. Aidha alisisitiza kuwa viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kushiriki katika vita dhidi ya ujangili kwani katika historia ya uumbaji, viumbe wote ni sawa na hamna mwenye dhamana ya kutoa uhai wa kiumbe kingine bila utaratibu maalum.

Katika hotuba yake, Askofu Munga alisema suala la uhifadhi linahitaji ushirikiano baina ya serikali na sekta nyingine. Hivyo, viongozi wa dini wako kwenye nafasi nzuri ya kutoa elimu ya uhifadhi kwa waumini wao. Alitoa rai ya kuunda mkakati utakaowezesha Wizara na Viongozi wa dini kubadilishana mawazo na elimu juu ya uhifadhi ili waumini wote waweze kupata elimu hiyo na hivyo kupunguza vitendo vya ujangili vinavyoendelea nchini.

Askofu Paul Shemsanga mwakilishi wa madhehebu ya Pentekosti naye aliongeza kuwa viongozi wa dini wana uwezo wa kubadili mitazamo na mawazo ya waumini wao kwa kuzingatia maadili ya kidini wanayofundishwa, jambo ambalo ni muhimu katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi.

Mhe Balozi Khamis Kagasheki alisema elimu ya uhifadhi ni muhimu kwa wananchi na aliwashukuru sana viongozi wa dini kwa kujitolea kusaidia katika hilo. Vilevile alisema sheria mbalimbali za uhifadhi zilizotungwa hazijitoshelezi iwapo wananchi ambao ndio walengwa hawazifahamu, hivyo kupitia viongozi wa dini na mikakati itakayoundwa, elimu ya sheria itawafikia wananchi wengi nchini.

Wizara ya Maliasili na Utalii imeridhia kuteua wajumbe watakaoungana na wajumbe kutoka kamati ya viongozi wa dini ili kupata timu itakayohusika na shughuli ya kuhakikisha ushirikiano wa elimu ya uhifadhi unafanyika baina ya pande hizo mbili.  

No comments:

Post a Comment