Social Icons

Saturday, 1 February 2014

KESHO NI SIKU YA ARDHIOEVU DUNIANI


Tarehe 2 Februari ya kila mwaka hufanyika maadhimisho ya siku ya ardhioevu duniani. Ardhioevu ni maeneo ya mabwawa, mbuga ya kinamasi, ardhi ya mboji au maji, yawe ya asili kutengenezwa na binadamu, ya kudumu au ya muda, yenye maji yaliyotuama au yanayotiririka, maji ya baridi au chumvi, ikiwa ni pamoja na maeneo ya maji ya bahari ambayo kina chake katika maji kupwa hakizidi mita sita. 
Maadhimisho haya huambatana na shughuli mbalimbali zinazolenga kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya umuhimu na faida za ardhioevu na mkataba wa kimataifa wa ardhioevu (Ramsar Convention) ambao Tanzania imeridhia mwaka 2000. 
Lengo la serikali kuridhia mkataba huu nikuhakikisha kuwa rasilimali za ardhioevu zinatumika kwa busara. Kauli mbiu ya siku ya ardhioevu mwaka huu 2014 ni; Sekta za Ardhioevu na Kilimo Kushirikiana ili Kuleta Maendeleo “Wetlands and Agriculture Partners for Growth". Kauli mbiu hii inatukumbusha umuhimu na jinsi ambavyo maendeleo ya sekta ya maji na kilimo hutegemea ardhioevu. 

Kwa sasa Tanzania imeorodhesha ardhioevu nne zenye umuhimu wa kimataifa. Ardhioevu hizo ni:- Bonde la mto Kilombero (kilomita za mraba 7, 950sq km) eneo hili ni makazi ya 75% Puku duniani; Malagarasi Muyovosi (kilomita za mraba 32,500) ambalo ni makazi ya ndege adimu aina ya Korongo nyangumi (Shoebill) na Mana (Wattled Crane); Ziwa Natron (kilomita za mraba 2,250) ambalo ni makazi kwa ndege aina ya Heroe mdogo (lesser flamingo); na Rufiji- Mafia -Kilwa (kilomita za mraba 5,970) kulinda rasilimali ya bahari ikiwepo Mikoko na Nguva.

UMUHIMU WA ARDHIOEVU
Kuna faida nyingi ambazo jamii pamoja na nchi hupata ikiwa rasilimali za ardhioevu zitatumika kwa busara. Ardhioevu ni chanzo kikubwa cha maji yanayotumika kwa; kilimo cha umwagiliaji, maji ya kunywa na matumizi mengine ya nyumbani, kunyweshea mifugo na Wanyamapori. Ardhioevu pia hutumika kwa shughuli za uvuvi wa samaki na utalii. Aidha, ardhioevu huzuia mafuriko na huchuja maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali pia ni chanzo muhimu cha maji yanayotumika kuzalisha nishati ya umeme.

ATHARI ZA MATUMIZI HOLELA YA ARHIOEVU
Kuna athari nyingi ambazo nchi itapata endapo ardhioevu zitaharibiwa. Mojawapo ya athari hizo ni; kukosa maji kwa ajili ya kumwagia mashamba wakati wa kiangazi na hatimaye kusababisha baa la njaa, kukosa samaki kwa jamii ya wavuvi, hivyo kusababisha ongezeko la umaskini na utapiamlo, uhaba wa maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo, wanyamapori na kupoteza pato la mtu mmoja mmoja, jamii na nchi kwa ujumla. Uhaba wa maji husababisha magonjwa ya mlipuko na kufa kwa viumbe maji wakiwemo samaki, viboko na mamba. Kwa ujumla athari hizi huleta mabadiliko ya kiikolojia yanayosababisha kutoweka kwa baioanuwai.

CHANGAMOTO ZA MATUMIZI YA ARDHIOEVU
Kilimo kisichofuata taratibu na kanuni zake ni chanzo cha kuharibika kwa ardhioevu. Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, hairuhusu mtu yeyote kulima mazao ndani ya mita sitini kutoka kwenye chanzo cha maji kwa mfano:- mto, ziwa, chem chem, bwawa n.k. Sheria hii imekuwa ikivunywa mara kwa mara.
Ufugaji wa mifugo wengi kuliko uwezo wa maeneo husababisha uharibifu wa mazingira kwa kutumia majani yote, kuacha ardhi wazi na hatimaye kusababisha maji ya mvua kupotea kwa wingi bila ya kuhifadhiwa kwenye ardhioevu ili iweze kuchuruzika kidogokidogo wakati wa kiangazi. Hii husababisha maji kuwa kidogo na vyanzo vya maji kukauka. Hali inaendelea kujitokeza katika ardhioevu karibu yote nchini. Ni vyema wafugaji wajitahidi kuwa na mifugo sawa na uwezo wa malisho.
Utupaji taka ovyo katika maeneo ya ardhioevu nalo limekuwa ni tatizo kwa jamii yetu. Wakati maeneo ya ardhioevu yamekuwa yakisaidia kusafisha maji kabla ya matumizi ya binadamu na wanyama, utupaji taka husababisha maeneo haya kuchafuka na kuharibika. Kwa mfano, asilimia hamsini (50%) ya ardhioevu nchini zimeharibiwa na asilimia tisini (90%) zimechafuliwa.


KAZI ZILIZOFANYIKA
Ili kuboresha Usimamizi Endelevu wa Ardhioevu Wizara ya Maliasili na Utalii imeandaa miongozo mbalimbali. Miongozo hiyo imeandaliwa ili kusaidia wanachi waliopo kandokando mwa ardhioevu kuendelea kutumia rasilimali za ardhioevu kwa uendelevu. Miongozo hiyo ni pamoja na:-
• Mwongozo kuhusu Utawala na Usimamzi wa Fedha kwa ajili ya programu ya uhifadhi na matumizi endelevu ya Ardhioevu. Mwongozo huu unazingatia dhana ya Serikali ya ugatuaji madaraka kwa jamii katika usimamizi wa raslimali za Maliasili na hutumika katika mchakato wa uandaaji wa mipango, bajeti na taarifa kulingana na mwongozo wa mpango wa muda mrefu wa taifa wa uandaaji mipango na bajeti;
• Mwongozo wa usimamizi wa matumizi endelevu ya rasilimali za Uvuvi ndani ya ardhioevu;
• Mwongozo wa usimamizi wa matumizi endelevu ya rasilimali maji (Kilimo cha umwagiliaji);
• Mwongozo wa usimamizi wa matumizi endelevu ya rasilimali za Wanyamapori;
• Mwongozo wa usimamizi wa matumizi endelevu ya rasilimali za mifugo ndani na karibu na maeneo ya ardhioevu;
• Mwongozo wa kutathmini na kutambua rasilimali za ardhioevu; na
• Kitabu kiongozi cha uhifadhi wa Ardhioevu nchini Tanzania.
Miongozo hii inakusudia kujenga uwezo kwa kuwapatia elimu wananchi wote kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya ardhioevu nchini. Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Malihai Clubs of Tanzania (MCT) pia imekuwa ikitoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa vijana wetu wa shule za msingi, sekondari pamoja na vyuo.
Hadi sasa serikali ikishirikiana na wafadhili imetekeleza miradi mbalimbali. Miradi hiyo ni pamoja na; usimamizi wa matumizi endelevu ya rasilimali za ardhioevu ambao umetekelezwa katika mikoa mitano ya Arusha, Iringa, Mbeya Kigoma na Tabora. Mradi huu uliokuwa wa manufaa makubwa katika kuanzisha maeneo manne ya Ramsar, maeneo ya uhifadhi wa jamii za wanyamapori kama vile Mawima na Isawima zinazozunguka eneo la Ramsar la Malagarasi Muyovosi, Jumuiya za wafugaji katika Mkoa wa Arusha wilaya za Longido na Ngorongoro, jumuiya za wavuvi katika mkoa wa Iringa/Njombe katika wilaya za Iringa vijijini, Makete, Njombe, Mufindi, Kilolo na Ludewa na Jumuiya za matumizi ya maji katika wilaya za mkoa wa Mbeya za Mbeya vijijini, Chunya, Mbozi na Mbarali. Aidha, serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuingiza usimamizi na matumizi endelevu wa rasilimali za ardhioevu kwenye Mipango ya Maendeleo ya Wilaya zilizotekeleza mradi wa Matumizi endelevu wa rasilimali za ardhioevu. Pia, serikali ipo kwenye maandalizi ya mkakati wa usimamizi wa matumizi endelevu ya rasilimali za ardhioevu nchini pamoja na kanuni.
Serikali pia inatekeleza mradi wa "Kilombero and Lower Rufiji Valley Wetlands Management Programme" (KILORWEMP) iliyoanza mwaka 2013 na utadumu kwa miaka mitano. 
Lengo la mradi huu ni kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali za ardhioevu ndani ya bonde la Mto Kilombero. Mradi huu unatekelezwa katika wilaya za Ulanga, Kilombero na Rufiji kwa ufadhili wa serikali ya Ubelgiji. 
Mradi utasaidia jamii pamoja na mambo mengine; kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Rasilimali za Ardhi (Land Use Management Plans) za wilaya na vijiji, Mipango Mikakati ya Usimamizi wa Rasilimali (Strategic Management Plans) na Mipango ya Jumla ya Usimamizi wa Rasilimali (General Management Plan) za wilaya husika.

Wito unatolewa kwa wananchi wote hasa wale wanaoishi karibu na maeneo ya ardhioevu kutunza maeneo haya. Aidha, wanashauriwa, kwa kushirikiana na wataalamu kutumia miongozo hii ili kujenga uwezo wa uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali hizi. 
Taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali ambao ni wadau wa uhifadhi wa ardhioevu wanashauriwa kuwajengea wananchi uwezo wa kuhifadhi na kutumia rasilimali za ardhioevu. Pia tutumie siku hii kuwa chachu ya kuhifadhi ardhioevu kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye.

TUTUNZE ARDHIOEVU ILI TUENDELEE KUFAIDI RASILIMALI ZAKE
</

No comments:

Post a Comment