Social Icons

Monday, 7 April 2014

ASKARI TOKOMEZA UJANGILI WASOTEA POSHO


Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu.
 
Askari  walioshiriki katika Operesheni Tokomeza Majangili, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete, kuingilia kati ili walipwe madai yao ya posho zinazofikia Sh. bilioni 1.5.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na NIPASHE, askari hao ambao majina yao yamehifadhiwa, walisema mpaka sasa hawajalipwa stahili zao na haijulikani watalipwa lini na serikali.

Walisema baada ya kuwasilisha madai yao, waliambiwa watalipwa fedha hizo ifikapo Desemba, mwaka jana, lakini mpaka sasa bado hawajalipwa.

“Katika zoezi hilo, tulishiriki askari 2,000, lakini kila tukizungumza na wenzetu, bado hakuna dalili tutalipwa lini,” alisema mmoja wa askari hao.

Walifafanua kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, aliahidi kuwa watalipwa malipo yao, lakini mpaka sasa hakuna kinachofanyika.

Aidha, walisema madai hayo ni fedha iliyoidhinishwa na Bunge ili walipwe, ikiwa ni posho ya kujikimu kwa muda waliokaa katika operesheni hiyo.

“Kama posho ziliidhinishwa na Bunge zilienda wapi? Hii tabia ya kutowalipa wafanyakazi baada ya kufanya kazi imekuwa ikijitokeza kwa viongozi wengi katika utumishi wa umma,” walisema.

Walimuomba Rais Kikwete kuliangalia suala hilo ili kujenga imani na viongozi wa nchi yao.

“Tunaomba kujua fedha zetu zitalipwa lini maana tunaona kimya cha muda mrefu au tumechinjiwa baharini?,”  Alihoji askari mwingine.

Akitoa ufafanuzi kuhusu madai hayo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa, alithibitisha serikali kudaiwa fedha hizo na kusema kwa sasa hali ya fedha siyo nzuri.

Aliwataka askari hao kuwa na subira ili kuipa nafasi serikali iendelee kujipanga na kukusanya fedha kwa ajili ya kuwalipa.

“Nadhani wanajua njia za kudai madai yao, ni vyema wafike wizarani ndiyo watapata jibu wanalipwa lini,” alisema Mgimwa.
 
CHANZO: NIPASHE
You might also like:     

No comments:

Post a Comment