Social Icons

Wednesday, 2 April 2014

SOMA: RISALA YA KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA TAIFA YA KUPANDA MITI MWAKA 2014Ndugu wananchi
Kama tunavyofahamu Tarehe Mosi Aprili kila mwaka ni SIKU YA TAIFA YA KUPANDA MITI. Maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Kupanda Miti yalifanyika kwa mara ya kwanza tarehe Mosi Januari mwaka 2001 kutokana na Waraka wa Waziri Mkuu Namba 1 wa mwaka 2000 ambao ulimtaka kila mwananchi kupanda miti kwa manufaa yake na kwa jamii kwa jumla.
Baadaye Waziri Mkuu alitoa Waraka mwingine Namba 1 wa Mwaka 2009, uliobadilisha Siku ya Taifa ya Kupanda Miti kuwa tarehe Mosi Aprili kila mwaka badala ya Januari Mosi. Hii ni kwa kuwa mwezi Aprili ni mwezi ambao sehemu nyingi nchini zinapata mvua, hivyo ni wakati muafaka wa upandaji miti.
Kama tunavyofahamu tarehe Mosi Aprili ni siku ya uhamasishaji pamoja na kupanda miti michache kama sehemu husika haitakuwa na mvua za kutosha kipindi hicho. 
Kama kawaida, kila mkoa umeandaa siku ya kupanda miti mingi zaidi kimkoa kufuatana na majira ya mvua katika mkoa husika. Pamoja na kupanda miti, siku hii pia inasisitiza utunzaji na uendelezaji wa msitu iliyopo hasa ile ya asili.
Ndugu wananchi
Maadhimisho ya mwaka huu napenda yawe ya kutafakari mchango wa kila mmoja wetu katika kutekeleza dhana ya kupanda miti kibiashara kwa matumizi endelevu ili misitu iwahudumie watu wa kizazi hiki na vijacho. Hii ina maana, upandaji wa miti sasa uchukuliwe kama kilimo cha mazao mengine ya biashara.
Tukumbuke kuwa MISITU YETU NDIO UHAI WETU hii ina maana kwamba mahitaji mengi muhimu ya maisha yetu ya kila siku yanategemea uwepo wa misitu kwa njia moja au nyingine.
Ndugu wananchi
Tanzania ina misitu inayokadiri wa kuwa na ukubwa wa hekta milioni 48 ambayo ni kama asilimia 55 ya eneo la ardhi la Tanzania Bara. Misitu hii inamilikiwa kama ifuatavyo:
• Hekta milioni 15.84 (35%) na Wakala wa Huduma za Misitu – Serikali Kuu; 
• Hekta milioni 3.36 (7%) Serikali za Mitaa 
• Hekta milioni 21.6 (45%) inamilikiwa na Serikali za Vijiji
• Hekta milioni 3.36 (7%) ikimilikiwa na sekta binafsi 
• Hekta milioni 2.4 (5%) ni misitu iliyo kwenye ardhi ya jumla (general land) na
• Takribani hekta 480,000 (1%) iko chini ya miliki zingine kama vile za kijadi kwa ajili ya matambiko na ibada za jadi.
Takwimu hizi zinabaini kuwa, ushiriki wa sekta binafsi kwenye kumiliki misitu ni mdogo sana. Kuna haja kubwa sasa, wadau wetu waongeze nguvu kwenye kumiliki misitu binafsi kama makampuni, mashirika, vikundi au watu binafsi. Sera na Sheria za Misitu zinaruhusu jambo hili.
Ndugu wananchi
Serikali kwa upande wake inashiriki kwa kufungua mashamba mapya ya miti. Kwa mfano, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Machi 24, mwaka huu ulianzisha shamba jipya la miti lenye ukubwa wa takriban hekta 12,000 katika eneo la Mbizi, karibu kabisa na Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa.
Ikumbukwe kuwa, ongezeko la watu Tanzania kutoka watu 22,455,193 mwaka 1988 hadi watu takriban 45 milioni mwaka 2013 ni ishara tosha kuwa kuna ongezeko pia la mahitaji ya mzao misitu. Ingawa misitu inaonekana kuchukua eneo kubwa la nchi hali yake si nzuri hata kidogo. Hali hii inaweza kulinganishwa na mtu aliyevaa nguo zilizochaa kwa nia ya kujistri! Misitu yetu ipo hoi!
Kwa ujumla wake misitu inakua kwa mita za ujazo milioni 83 ambapo kati ya hizo mita za ujazo 41 zipo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kama vile misitu ya hifadhi ya Lindimaji (catchment forests) na misitu iliyopo kwenye maeneo ya hifadhi za wanayapori. Kisheria hairuhusiwi kuvuna katika misitu hii. Kwa mantiki hiyo basi, kiasi cha mita za ujazo milioni 42 ndizo tunaruhusiwa kuvuna kwa mwaka.
Ndugu wananchi
Mahitaji ya nchi ya mazao ya misitu ni mita za uzazo milioni 62 kwa kila mwaka. Hivyo basi ukilinganisha kiasi tunachotakiwa kuvuna kiundelevu na mahitaji ni dhahiri kuwa kuna pengo la mita za ujazo milioni 20 kwa mwaka. Pengo hili ndilo linalosababisha wizi wa mazao ya mizitu na uvunaji katika misitu isiyoruhusiwa..
Ndio maana Ndugu wananchi Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania wanawahamasisha wadau mabilimbali kushiriki kikamilifu katika juhudi unapandaji miti na kufungua mashamba mapya ya miti na kupanua maeneo ya upandaji miti kwenye mashamba ya zamani, ili kukidhi mahitaji yetu bila kuathri mazingira ya nchi yetu.
Ni wito wangu kuwa, sekta binafsi ijihusishe zaidi katika kupanda miti kibiashara ili kuziba au kupunguza pengo hili.
Mkoa wa Njombe ni moja ya mikoa yenye muitikio mkubwa wa sekta binafsi kujihusisha kwenye upandaji miti kibiashara. Serikali inaziona juhudi hizi, ingawa fursa za kuzalisha zaidi bado hazijatumika kikamilifu.
Napenda kuwasihi wadau wa mkoa wa Njombe na wengine nchini kote kuongeza uzalishaji wa raslimali za misitu ili kuyafanya maisha hapa duniani kuwa bora na sio bora maisha!
Sera ya Taifa ya Misitu, inahimiza ushiriki wa sekta binafsi kwenye kupanda miti na kuitunza ili kuchangia kwenye pato la Taifa, kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuhakikisha viwanda vyetu vya misitu vinapata malighafi kwa kiwango kinachohitajika.
Ndugu wananchi,
Ningependa kuchukua fursa hii kuwapongeza wananchi ambao wanastawisha miche na kuipanda. Napenda pia kuwapongeza na kuwatia moyo wale wote wanaomiliki misitu ya asili na ile ya kupandwa kwa lengo la kuhifadhi mazingira na pia kuitumia katika kuongeza kipato na kuitumia kwa mahitaji yao binafsi au ile ya jamii.
Ili kufanikisha upandaji miti nchini, natoa wito kwa kila familia kuanzisha bustani za miche watakayoimudu ili pia kuwa na mashamba yao ya miti watakayomudu kuyasimamia.
Ndugu wananchi
Baada ya kusema hayo, nawatakia wananchi wote maadhimisho mema ya Siku ya Taifa ya Upandaji Miti mwaka 2014.
MISITU NI UHAI, PANDA MITI KWANZA NDIPO UKATE MTI
Katibu Mkuu
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII


No comments:

Post a Comment