Social Icons

Sunday, 11 May 2014

TAARIFA KWA WATU WOTE: MKURUGENZI WA IDARA YA WANYAMAPORI PROFESA NGASONGWA HAJAWAHI KUFUKUZWA KAZI AMA KUADHIBIWA.

Serikali inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa potofu zinazoendelea kuchapishwa na kutangazwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuhusu Watumishi Waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexander Songorwa ambaye ni Mkurugenzi, Idara ya Wanyamapori na Prof. Jafari Kideghesho, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori. 

Kumekuwa na taarifa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kwamba Wakurugenzi hao walikuwa wamefukuzwa kazi na Waziri wa Maliasili na Utalii, na kisha kurejeshwa kwa maelekezo ya Ikulu. Taarifa hizo si sahihi. 

Ukweli ni kwamba Prof. Alexander Songorwa na Prof. Jafari Kideghesho hawajawahi kufukuzwa kazi ama kuadhibiwa. Hatua za kinidhamu katika Utumishi wa Umma zina taratibu na miongozo yake, inayotawaliwa na nyaraka kuu nne, miongoni mwa nyingine, kama ifuatavyo:
  •   Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 1999;
  •   Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa
    mwaka 2008);
  •   Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003;
  •   Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009.
    Kwa mujibu wa nyaraka hizo, na kwa mujibu wa sheria, kila mtumishi wa umma anayo mamlaka yake ya ajira na mamlaka yake ya nidhamu.
    Mamlaka ya nidhamu ya Prof. Alexander Songorwa na Prof. Jafari Kideghesho haijawahi kuwachukulia hatua zozote za kinidhamu. Lakini, baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii kuonyesha kutoridhika na utendaji wao, Mamlaka yao ya nidhamu iliwaruhusu kuchukua likizo zao za mwaka za kawaida. Likizo zao zilipoisha walirejea kazini kama kawaida. 
Hata hivyo, kutokana na yaliyokwisha kutokea, wanataaluma hawa, Prof. Alexander Songorwa na Prof. Jafari Kideghesho, kwa hiari yao wenyewe, wamekubali kuchukua majukumu mengine katika Utumishi wa Umma kama watakavyopangiwa.
Serikali inapenda kukumbusha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameunda Tume ya Uchunguzi kuhusu utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Miongoni mwa hadidu za rejea za Tume ni kubainisha kila aliyefanya kosa wakati wa kutekeleza Operesheni Tokomeza na kupendekeza hatua stahiki dhidi ya wahusika. Serikali inashauri Tume ipewe nafasi ya kukamilisha kazi yake ndipo tutajua mkosaji ni nani na anastahili kuchukuliwa hatua gani. Serikali inaomba pia kila mwenye taarifa na ushahidi utakaoisaidia Tume aifikishe kwao.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO 
Dar es Salaam, 10 Mei, 2014 

No comments:

Post a Comment