Social Icons

Friday, 9 May 2014

TAARIFA: MAADHIMISHO YA SIKU YA NDEGE WAHAMAO DUNIANI TAREHE 10 – 11 MEI 2014


031
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII 
TAARIFA KWA UMMA
MAADHIMISHO YA SIKU YA NDEGE WAHAMAO DUNIANI
TAREHE 10 – 11 MEI 2014 
Maadhimisho ya Siku ya Ndege Wahamao Duniani ni siku  ambayo huadhimishwa kimataifa kila mwaka tarehe 10 na 11 Mei.
Wizara ya Maliasili na Utalii inawashauri wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya Ardhi oevu ambayo ni makazi na mapito ya ndege wahamao kushirikiana na Serikali katika kuwalinda ndege hao na kuhifadhi mapito na makazi yao.Wananchi pia wanakumbushwa kuwa maeneo ya ardhioevu ndio vyanzo vya maji ambayo yanafaa kwa matumizi ya kila siku ya binadamu, wanyama na ndege, hivyo maeneo hayo ni vyema yalindwe kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Kuna aina nyingi za ndege maji na wahamao. Aina za ndege hao ni kama vile Heroe mkubwa na mdogo (flamingos) ambao wanahama kila mwaka kutoka sehemu moja ya dunia kwenda nyingine kutafuta malisho, maji, kukwepa hali mbaya ya hewa na kupata sehemu salama ya kuzaliana.
Tanzania ni nchi mojawapo yenye sehemu nyingi ambazo ni salama kwa mazalia ya ndege. Kwa mfano, Ziwa Natron ni maarufu kwa mazalia ya ndege aitwaye Heroe mdogo. Inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya Heroe mdogo kote duniani huzalia katika Ziwa Natron liliko Kaskazini mwa Tanzania.   Ziwa hilo ni kivutio cha utalii kutokana na ndege, wanyamapori na mandhari ya Ziwa.
Maadhimisho ya Siku ya Ndege Wahamao Duniani yalianza mwaka 2006 na kuendelea kusherehekewa kila mwaka mwishoni mwa wiki ya pili ya kila mwezi Mei.  Watu duniani kote huitumia fursa hii kutoa elimu na kufanya matembezi katika sehemu zenye Ndege hawa  kwa ajili ya kusherehekea siku hii. Kwa mwaka huu Wizara ya Maliasili itafanya maadhimisho hayo Katika Eneo la Ramsar la Ziwa Natron lililopo Mkoani Arusha. Eneo hili lina umuhimu wa ndege wahamao aina ya Heroe mdogo.
Ujumbe wa mwaka huu wa Siku ya Ndege Wahamao ni: “Mahali Wanapofikia Ndege Wahamao na Utalii (Destination Flyways; Migratory Birds and Tourism), “. Tafsiri ya ujumbe huu ni kuwa nchi, mashirika na watu binafsi wanatakiwa kutunza maeneo wanapolazimika kufikia ndege wahamao kwa kila mwaka kwa ajili ya uhifadhi endelevu wa ndege hao pamoja na kusaidia jamii kutambua umuhimu wa ndege hao katika kuvutia utalii.
Utunzaji wa ndege wahamao ni sababu mojawapo iliyofanya Tanzania kusaini Mkataba wa Uhifadhi wa Ardhioevu (Ramsar) mwaka 2000. Ardhioevu, pamoja na maufaa mengine ikiwepo maji, chakula, kurekebisha hali ya hewa, kusafisha maji machafu na kuzuia mafuriko pia ni makazi ya wanyamapori wakiwemo ndege wahamao.
Kutokana na Mkataba huo Tanzania imetenga maeneo ya Ramsar ambayo ni muhimu katika kuhifadhi bioanuwai. Maeneo ya ardhioevu yaliyotengwa hususani kwa uhifadhi wa ndege ni pamoja na Ardhioevu zenye umuhimu wa kimataifa kama vile:- Malagarasi-Muyovozi ambayo ni muhimu kwa uhifadhi wa ndege aina ya Korongo domokiatu (Shoebill stork), na eneo la Ramsar la Ziwa Natron ambalo ni muhimu katika kuhifadhi  ndege aina ya Heroe mdogo (lesser flamingo).
Serikali imekuwa ikiwajengea wananchi uwezo wa kuhifadhi na kutumia rasilimali za ardhioevu nchini kwa kutoa elimu ya uhifadhi katika maeneo yanayozunguka maeneo ya Ramsa. Maeneo hayo ambayo ni makazi muhimu ya ndege wahamao yanasimamiwa na Sheria ya Kuhifadhi Mazingira ya mwaka 2004 na ya Kuhifadhi Wanyamapori ya Mwaka 2009.
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
9 Mei 2014

No comments:

Post a Comment