Social Icons

Tuesday, 18 August 2015

UJANGILI WATISHIA KUDHOOFISHA UKUAJI WA SEKTA YA UTALII


Na Mwandishi Wetu
UJANGILI uliokithiri nchini Tanzania unatishia kudhoofisha uchumi wa nchi ambao unazidi kukua kutokana na sekta ya utalii kuwa na mchango mkubwa kwenye pato la taifa na katika kuongeza ajira. 

Dk. Adelhelm Meru, Katibu Mkuu wa Wizara ya maliasili na utalii, ameonya kwamba kuna uwezekano ujangili ukaathiri ajira zipatazo milioni 3.8 kwenye sekta ya utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki wakiwemo waongoza watalii, madereva, mahoteli pamoja na wahudumu wa migahawa. 

Kwa mujibu wa shirika la All Africa Tanzania pamoja na nchi nyingine barani Afrika zimeathirika sana kutokana na ujangili katika miaka kumi iliyopita. Mwaka jana utafiti ulionyesha kuwa Tanzania imepoteza zaidi ya nusu ya tembo wake ambapo idadi imepungua kutoka tembo 110,000 mwaka 2009 kufikia chini ya tembo 44,000. Twiga pia ambao ni alama ya taifa nao wamepungua kwa kiasi kikubwa.

Meru amesema kuwa japo majangili wanazidi kunufaika na biashara hii, sekta ya utalii inaendelea kuumia. Amesema Tanzania ina ajira 700,000 kutokana na utalii na anasema idadi hiyo ya ajira inaweza kuongezeka mara mbili endapo ujangili uliokithiri kwa wanyamapori utaisha. 

Katika kuisaidia serikali ya Tanzania hivikaribuni, mashirika ya Wildaid na African Wildlife Foundation yalizindua kampeni mpya ijulikanayo kama “Ujangili Unatuumiza Sote” kwa kushirikiana na wizara ya maliasili na utalii. Kampeni hii inatumia viongozi wa dini na watu maarufu katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu janga la ujangili na pia kuwakumbusha Watanzania kulinda wanyamapori ambao ni fahari na rasilimali kubwa kwa taifa. 

Kampeni hii itatumia runinga, redio, mitandao ya jamii, magazeti, vijarida, matangazo na filamu zitakazoonyeshwa kwenye maeneo ya wazi ili kuwafikia wananchi waishio mijini na vijijini. 

Utafiti uliofanywa na WildAid kwa kushirikiana na African Wildlife Foundation kwa Watanzania kwa kuwahoji Watanzania zaidi ya 2,000 waishio mijini na vijijini uligundua kwamba asilimia 80 kati yao wanaelewa madhara yanayoweza kuikumba Tanzania endapo tembo watatoweka. Kati ya walihojika katika utafiti huo, asilimia 73 walisema kwamba wanyama pori ni mojawapo ya alama za taifa na urithi wa taifa. 

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Wildaid, Peter Knights amesema kwamba "Ujangili kwa tembo ni wizi unaowaumiza Watanzania wa sasa na wa vizazi vijavyo. Tunaviomba vyombo vya habari kushiriki katika kampeni hii na tunahitaji kila mmoja asaidie katika mapambano kukomesha ujangili”.

Chanzo Mtaa kwa Mtaa Blog No comments:

Post a Comment