Social Icons

Thursday, 12 November 2015

Serikali imeombwa kulinda usalama wa Tembo‏Na Mwandishi wetu – Maelezo
Serikali imeshauriwa  kuiomba China kutekeleza ahadi yake ya kufunga masoko yote ya meno ya Tembo  ili kuweza kulinda usalama wa muda mrefu wa wanyama  hao kwani nchi hiyo  ni mtumiaji mkubwa wa meno hayo na kwa  kufunga biashara hiyo kutapelekea  kuanguka kwa haraka kwa biashara katika sehemu nyingine ulimwenguni.

Ombi hilo limetolewa leo na Taasisi  inayopinga uwindaji haramu wa tembo wakati wakisoma barua yao ya wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari uliopo jijini Dar es Salaam.

Akisoma barua hiyo Shubert Mwarabu ambaye ni mratibu wa kampeni ya okoa Tembo wa Tanzania alianza kumpongeza Mhe. Rais kwa kuchaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano na kuisihi Serikali  kutumia urafiki wa kihistoria kati yake  na China kufunga masoko ya meno ya Tembo yaliyopo nchini China.

Alisema takribani asilimia 90 ya meno ya Tembo toka Tanzania yanauzwa China, ambapo biashara halali ya meno ya Tembo inatumika kama mwavuli wa biashara haramu ya meno ya Tembo ambacho ndio chanzo kikuu cha tatizo la ujangili wa Tembo.

“Tunakuandikia barua leo kukuomba kuchukua hatua juu ya suala la kupungua kwa kasi idadi ya Tembo nchini kutokana na ujangili kwa ajili ya biashara haramu ya meno ya Tembo”.

“Kutokana na Ripoti ya Sensa ya TAWIRI 2014 Miaka hamsini iliyopita, kulikuwa na Tembo 300,000 nchini Tanzania. Mwaka 2009, kulikuwa na Tembo 109,000. Leo, inakadiriwa kuna Tembo 43,000 tu waliobaki – upungufu wa asilimia 60 ndani ya miaka mitano tu”, alisema Mwarabu.

Aliendelea kusema wanatambua hatua zilizofanyika kukabiliana na tatizo la ujangili. Uundaji wa mikakati ya kitaifa dhidi ya ujangili, juhudi za Kikosi Kazi cha National and Transnational Serious Crimes Investigation Unit (NTSCIU) na kuongeza rasilimali kwa mamlaka ya wanyamapori ni hatua muhimu.

Alisisitiza, “Nchi yetu imekuwa mstari wa mbele katika uhifadhi wa Tembo hapo kabla. Mwaka 1989, Tanzania iliongoza jitihada za kupiga marufuku biashara ya meno ya Tembo ulimwenguni tulipochukua hatua kukomesha mauaji ya Tembo, dunia nzima ilituunga mkono. Ni lazima turejeshe upya dhamira yetu kwa ahadi tuliyojiwekea kwa hatua ya kimataifa zaidi ya miaka ishirini iliyopita, na kuleta ukomo wa biashara yote ya meno ya Tembo”.

“Tunaiomba serikali kuwakamata na kuwashitaki wafanyabiashara wakubwa wa meno ya Tembo nchini, bila kujali utaifa, hadhi au mamlaka, kuteketeza hadharani ghala ya meno ya Tembo Tanzania – inayosadikika kuwa kubwa kuliko yote ulimwenguni kwani ni gharama kutunza na kulinda ghala la meno ya Tembo Tanzania”.       

No comments:

Post a Comment